Zaidi ya magaidi 50 wauawa Sinai, Misri
Jeshi la Misri limetangaza kuwa, magaidi 52 wameuawa katika operesheni ya kijeshi iliyofanyika dhidi ya kundi moja la kigaidi katika mkoa wa Sinai Kaskazini.
Taarifa iliyotolewa leo na Komandi ya Jeshi la Misri imesema kuwa, magaidi 52 wameuawa katika opereheni hiyo na maficho 7 na magari yao 28 yameharibiwa.
Vilevile jeshi la Misri limefanikiwa kushika silaha za aina mbalimbali zilizokuwa mikononi mwa magaidi hao zikiwemo bunduki za rashasha, mabomu, bastola, mada za milipuko za TNT na pikipiki 52. Askari 3 wa jeshi la Misri pia wameuawa katika operesheni hiyo.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Jeshi la Misri limekuwa likifanya mashambulizi makubwa na ya pande zote dhidi ya maficho ya wanamgambo wa makundi ya kigaidi katika eneo la Sinai Kaskazini.
Kundi linalojiita Ansar Baitul Maqdis ambalo baada ya kuungana na kundi la Daesh limebadilisha jina na kjiita Wilaya ya Sinai, kwa miaka kadhaa sasa limekuwa likishambulia kambi na maeneo ya jeshi na polisi ya Misri na hadi sasa limeua makumi miongoni mwao.