Gaidi hatari zaidi wa Misri atiwa nguvuni Derna, Libya
Msemaji wa Jeshi la Taifa la Libya ametangaza kuwa, jeshi hilo limemtia nguvuni kinara wa makundi ya kigaidi katika mkoa wa Derna huko kaskazini mwa Libya.
Ahmed al-Mismari amesema kuwa, Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar limefanikiwa kumtia nguvuni Hisham Ashmawy, gaidi hatari zaidi wa Misri katika operesheni iliyofanyika mkoani Derna.
Al Mismari ameongea kuwa, kinara huyo wa makundi ya kigaidi atakabidhiwa kwa serikali ya Misri baada ya vyombo vya usalama vya Libya kukamilisha uchunguzi.
Hisham Ashmawy anayetambuliwa kuwa gaidi hatari zaidi wa kigeni nchini Libya anaongoza kundi linalojiita Murabituun lenye mfungamano na kundi la kigaidi la al Qaida huko Derna na amekuwa akiongozi harakati za kundi hilo tangu miaka minne iliyopita.
Ashmawy aliyewahi kuwa kamanda katika jeshi la Misri amehusika na mashambulizi mengi ya kigaidi yaliyofanyika nchini humo likiwemo lile lililomlenga waziri wa zamani wa mambo ya ndani wa Misri, Mohamed Ibrahim mwaka 2013.
Gaidi huyo aliyepata mafunzo nchini Marekani alikuwa afisa katika kikosi cha al Saaiqa cha jeshi la Misri. Baada ya kufukuzwa jeshini mwaka 2011 kutokana na misimamo yake ya kufuru mipaka, alianzisha kundi la kigaidi lililojumuisha pamoja wafuasi wa makundi ya kiwahabi na kitakfiri.