Waziri wa Nchi Tanzania: Rais Magufuli hakukusudia kupiga marufuku uzazi wa mpango
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) nchini Tanzania, Seleman Jafo amesema kuwa, wataalamu wa masuala ya afya wa nchi hiyo walitakiwa kuwafafanulia wananchi kauli ya Rais John Pombe Magufuli pale alipotaka Watanzania wasizuiwe kuzaa watoto.
Kwa mujibu wa Jafo ufafanuzi huo ungeisaidia jamii kupata uelewa kamili yale yaliyokusudiwa na Rais Magufuli. Aidha amebainisha kwamba, Rais Magufuli hakumaanisha watu wasifuate njia za uzazi wa mpango kama ilivyotafsiriwa. Seleman Jafo, ameyasema hayo Jumanne ya leo na kusisitiza kuwa, kauli ya Rais John Pombe Magufuli ililenga kuwataka watu wasipangiwe idadi ya watoto ila sio kuacha kabisa kutumia njia za uzazi wa mpango. "Hivi ni vitu viwili tofauti na nyie kama wataalamu wa afya mlitakiwa muonyeshe mfano kwa kuwaelewesha wananchi na sio kuwaacha wabaki na mtazamo hasi." Amesema Waziri Jafo.
Kadhalika amesema kuwa, taifa la Tanzania bado linaamini katika utumiaji wa njia za uzazi wa mpango kwa sababu unaboresha pia afya ya mama na mtoto. Havi karibuni Tanzania ilishuhudia mjadala kufuatia kauli ya rais wa nchi hiyo aliyewataka Watanzania wasiogope kuwa na watoto wengi na badala yake waendelee kuzaa kwa wingi, sambamba na kupuuza sera ya uzazi wa mpango. Katika uwanja huo asasi mbalimbali kikiwemo chama kikuu cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, waliwahamasisha wananchi kufuata uzazi wa mpango na kwamba hiyo ndio sera ya taifa hilo.