Kaburi la umati lagunduliwa Sirte, Libya, lina zaidi ya maiti 100
Vyombo vya usalama nchini Libya vimetangaza kuwa, vimegundua kaburi la umati lenye maiti za makumu ya watu lililoko umbali wa kilomita 15 magharibi mwa mji wa Sitre huko kakazini mwa nchi hiyo.
Kaburi hilo lina maiti za watu 110 na ripoti zinasema kuwa baadhi ya maiti hizo zina sare za jeshi na nyingine zimefungwa mikono.
Naibu mwanasheria wa mji wa Sirte, Abu Bakr Waniis amesema kuwa, maiti hizo zilizikwa eneo hilo miaka miwili iliyopita na kwamba uchunguzi wa kubaini utambulisho wao na jinsi walivyouliwa na kuzikwa katika kaburi moja utaanza haraka iwezekanavyo.
Katika kipindi cha wiki moja iliyopita kumegunduliwa makaburi matatu ya umati yenye maiti za watu 225 huko Sirte nchini Libya. Mji huo ulikuwa makao makuu ya kundi la kigaidi la Daesh tangu msimu wa machipuo wa mwaka 2015 hadi mwishoni mwa msimu wa mapukutiko wa mwaka 2016.
Libya ilitumbukia katika machafuko ya ndani ya ghasia kubwa zinazochochewa na makundi ya kigaidi baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddaf kwa msaada wa nchi za Magharibi wanachama wa NATO.