Polisi Tanzania: Waliomteka MO Dewji walihitaji tu fedha; mjadala waendelea mitandaoni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48928-polisi_tanzania_waliomteka_mo_dewji_walihitaji_tu_fedha_mjadala_waendelea_mitandaoni
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro amesema kuwa, watu waliomteka mfanyabiashara mkubwa wa nchi hiyo na Afrika Mohammed Dewji ‘MO’ walitaka kupewa fedha ingawa hakutaja kiwango hicho cha fedha walichokihitaji.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 20, 2018 12:54 UTC
  • Polisi Tanzania: Waliomteka MO Dewji walihitaji tu fedha; mjadala waendelea mitandaoni

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro amesema kuwa, watu waliomteka mfanyabiashara mkubwa wa nchi hiyo na Afrika Mohammed Dewji ‘MO’ walitaka kupewa fedha ingawa hakutaja kiwango hicho cha fedha walichokihitaji.

Sirro ameyasema hayo Jumamosi ya leo katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam ambako watekaji walimtupa bilionea huyo, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa kwa ajili ya kuwatia mbaroni wahalifu hao. Katika viwanja hivyo vya Gymkhana kumekutwa gari lililotelekezwa na ambalo limetajwa kuwa ndilo lilihusika na utekaji. Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro  amesema: “Hii gari imetelekezwa na Mohammed Dewji ameachiwa lakini yeye mwenyewe amesema wazi kuwa waliomteka waliomba fedha ila hawakusema ni kiasi gani.” Amesema Sirro. Kadhalika mkuu huyo wa Polisi Tanzania ameongeza kwa kusema: “Ila MO Dewji amesema  waliomteka walikuwa na wasiwasi na amesema kuwa walizungumza na baba yake (Gullam Dewji). Pia ameeleza jinsi walivyomchukua pale hotelini (Colosseum) na kumpeleka sehemu ambako walimfungia.”

Mohammed Dewji aliyekuwa ametekwa nyara na watu wasiojulikana na kuachiliwa leo

Ndani ya gari hiyo kumekutwa na silaha kadhaa zikiwemo bastola tatu, bunduki ya kivita aina ya AK 47 na risasi 19. Kamanda Sirro pia amewaonya watu waliotoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii wakikosoa maelezo aliyoyatoa jana kuhusu ulipofikia uchunguzi wa tukio la kutekwa kwa bilionea huyo. Hata hivyo kumeibuka mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii ambapo watu wamehoji iwapo watekaji waliweza kufika eneo la Gymkhana lenye ofisi muhimu za serikali wakiwa na gari lililotajwa kuhusika na uhalifu, kisha wakaweza kuondoka eneo hilo majira ya usiku bila kutiwa mbaroni. Kati ya watu waliohoji suala hilo ni pamoja na Maria Sarungi mwanaharakati maarufu wa upinzani nchini Tanzania ambaye ameandika: “Watanzania mna maswali magumu sana! Ila sasa majibu sina hata mimi kuna mtu ananiuliza baada ya watekaji kumtelekeza MO Dewji na gari pale Gymkhana karibu na Ikulu na ofisi nyeti za serikali pamoja na ubalozi, waliondokaje? Na Uber? Sina jibu mniacheee.”