Libya yalalamikia kufanyika kikao cha waungaji mkono wa Jenerali Haftar nchini Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48957-libya_yalalamikia_kufanyika_kikao_cha_waungaji_mkono_wa_jenerali_haftar_nchini_misri
Maafisa usalama wa serikali ya mwafaka wa kitaifa ya Libya wamelalamikia kufanyika kikao cha waungaji mkono wa Jenerali Khalifa Haftar, kamanda wa vikosi viitwavyo Jeshi la Taifa la Libya katika mji mkuu wa Misri, Cairo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 21, 2018 21:05 UTC
  • Libya yalalamikia kufanyika kikao cha waungaji mkono wa Jenerali Haftar nchini Misri

Maafisa usalama wa serikali ya mwafaka wa kitaifa ya Libya wamelalamikia kufanyika kikao cha waungaji mkono wa Jenerali Khalifa Haftar, kamanda wa vikosi viitwavyo Jeshi la Taifa la Libya katika mji mkuu wa Misri, Cairo.

Maafisa usalama wa serikali ya mwafaka wa kitaifa ya Libya wametoa indhari kuhusu malengo ya kikao hicho cha Cairo cha waungaji mkono wa Jenerali Haftar, na kueleza kwamba kila baada ya muda huwa kunafanyika vikao vya kutia shaka na wasiwasi kwa uungaji mkono wa serikali ya Misri ambayo upendeleo wake kwa kamanda huyo wa vikosi viitwavyo Jeshi la Taifa la Libya unajulikana wazi.

Kwa mujibu wa maafisa hao wa usalama wa serikali ya mwafaka wa kitaifa ya Libya, kufanyika vikao vya aina hiyo mjini Cairo ni kielelezo cha uingiliaji unaofanywa na nchi za eneo ikiwemo Misri katika masuala ya Libya ambao utashadidisha matatizo ya ndani ya nchi hiyo.

Hali ya mchafukoge ya kukosekana uthabiti na usalama iliyotokea karibuni katika mji mkuu wa Libya, Tripoli

Siku ya Jumatano iliyopita, idadi kadhaa ya maafisa wa kijeshi wanaomuunga mkono Jenerali Khalifa Haftar walifanya kikao mjini Cairo, Misri ambacho kilihudhuriwa pia na wawakilishi wa vyombo vya intelijensia na maafisa wa jeshi la nchi hiyo.

Maafisa wa serikali ya Misri hadi sasa wamenyamaza kimya na hawajatoa maelezo yoyote kuhusu malengo ya kikao hicho.

Tangu mwaka 2011, Libya iko kwenye hali ya mchafukoge ikishuhudia machafuko na mvurugiko wa uthabiti kutokana na uingiliaji kijeshi uliofanywa na Marekani na shirika la kijeshi la NATO.

Hivi sasa nchi hiyo ina serikali mbili; moja ikiwa ni ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al-Sarraj, ambayo inaungwa mkono na jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa, na nyingine iliyoko mji wa Tobruk mashariki mwa nchi hiyo, ambayo inamuunga mkono Jenerali Khalifa Haftar.../