Paul Biya atangazwa mshindi wa urais nchini Cameroon
Pau Biya, kiongozi wa zamani zaidi barani Afrika ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 7 mwezi huu wa Oktoba, kwa kupata asilimia 71 ya kura. Hayo yametangazwa na Baraza la Katiba la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Akitangaza matokeo rasmi ya uchaguzi huo wa Oktoba 7, mkuu wa baraza hilo, Clement Atangana amesema kuwa, Biya amepata asilimia 71.3 ya kura akifuatiwa kwa mbali na mgombea wa mrengo wa upinzani, Maurice Kamto aliyepata asilimia 14.2 ya kura.
Baraza hilo ambalo wajumbe wake wameteuliwa na Paul Biya, limetupilia mbali mashtaka yote ya wapinzani ya kulalamikia uchaguzi huo.

Wanajeshi wamemwagwa kwa wingi katika miji yote mikuu leo Jumatano na serikali imepiga marufuku maandamano yoyote ya wapinzani.
Wapiga kura walikuwa wachache katika uchaguzi huo kwenye maeneo yanayozungumza Kiingereza baada ya zaidi ya watu laki mbili kukimbia makazi yao kukwepa mapigano baina ya askari wa serikali na waasi wanaopigania kujitenga maeneo hayo.
Biya amepata asilimia 75 ya kura katika maeneo hayo yanayopigania kujitenga na Cameroon.
Itakumbukwa kuwa, Oktoba 9, mgombea wa chama cha upinzani cha Movement for the Rebirth of Cameroon (MRC), Maurice Kamto alijitangaza mshindi wa uchaguzi huo uliofanyika Jumapili ya tarehe 7 Oktoba.