Algeria na Mauritania zakutana kuzungumzia Sahara Magharibi
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Algeria na Mauritania wameitisha kikao cha pamoja cha kujadili hatima ya Sahara Magharibi inayopigania uhuru wake kutoka kwa Morocco.
Ismail Ould Cheikh Ahmed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritania na Abdolkader Massahel, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria wamekutana huko Nouakchott, mji mkuu wa Mauritania na kujadiliana kadhia ya Sahara Magharibi.
Horst Koehler, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika suala la Sahara Magharibi amezitaka Morocco, Algeria, Mauritania na harakati ya Polisario inayopigania uhuru wa Sahara Magharibi zikutane mjini Geneva Uswisi tarehe nne na tano Disemba mwaka huu ili kujadiliana kadhia hiyo.

Harakati ya Polisario imekuwa ikiendesha mapambano tangu mwaka 1973 ya kupigania uhuru wa Sahara Magharibi kutoka kwa Morocco.
Mapigano baina ya askari wa Morocco na harakati huo yalianza mwaka 1975 na yalisimama mwaka 1991 baada ya kufikiwa mapatano ya kusimamisha vita yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Serikali ya Morocco inapigania kulibakisha eneo hilo la Sahara Magharibi ndani ya mamlaka yake lakini harakati ya Polisario inapinga suala hilo na inataka kuitishwa kura ya maoni itakayotoa mwanya kwa wakazi wa eneo hilo kujiamulia wenyewe mustakbali wao wa imma kuwa na nchi yao huru au kuwa chini ya utawala wa Morocco.