Suitafahamu yaibuka kuhusu kuondoka balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49221-suitafahamu_yaibuka_kuhusu_kuondoka_balozi_wa_umoja_wa_ulaya_nchini_tanzania
Duru za habari nchini Tanzania zimeeleza kuwa, balozi wa Umoja wa Ulaya nchini humo, Roeland Van de Geer ameondoka nchi hiyo, huku ikielezwa kuwa huwenda amepewa notisi iliyomtaka kuondoka Tanzania.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 03, 2018 04:47 UTC
  • Suitafahamu yaibuka kuhusu kuondoka balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania

Duru za habari nchini Tanzania zimeeleza kuwa, balozi wa Umoja wa Ulaya nchini humo, Roeland Van de Geer ameondoka nchi hiyo, huku ikielezwa kuwa huwenda amepewa notisi iliyomtaka kuondoka Tanzania.

Kwa mujibu wa habari hiyo, Geer mabaye ni raia wa Uholanzi alitakiwa kuondoka ardhi ya nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufikia Novemba tatu ya leo ingawa hadi sasa serikali ya Dar es Salaam haijaweka wazi kadhia hiyo. Duru hizo zimebainisha kwamba, msaidizi wa balozi huyo, Charles Andrew-Stuart ndiye atachukua mikoba ya Roeland Van de Geer kwa muda, wakati hatua zaidi zikichukuliwa. Hii ni katika hali ambayo ubalozi wa EU nchini Tanzania umetangaza kwamba, Geer aliondoka nchi hiyo jana usiku kuelekea makao makuu ya umoja huo mjini Brussels, Ubelgiji kwa ajili ya kujadili masuala ya kisiasa yaliyojiri hivi karibuni nchini humo. Kwa mujibu wa msaidizi wa balozi huyo, Charles Stuart Geer ameitwa makao makuu mjini Brussels kwa majadiliano zaidi na ngazi za juu za kisiasa kuhusu matukio ya hivi karibuni nchini Tanzania.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania

Aidha ubalozi huo wa EU umesema kwamba, Roeland ameenda kukutana na maofisa wa ngazi za juu wa umoja huo kujadili pia ushirikiano wa baadaye kati ya umoja huo, wanachama wake na Tanzania. Alipoulizwa kuhusu suala hilo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Augustine Mahiga hakuwa tayari kulizungumzia, huku akisema kuwa atalitolea ufafanuzi baadaye. Roeland atakuwa balozi wa pili kuondoka Tanzania katika mazingira kama hayo kwenye miaka ya hivi karibuni baada ya Awa Dabo, wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) aliyeondoka Aprili mwaka jana. Hata hivyo, serikali ya Tanzania ilisema kuwa Dabo aliondolewa kutokana na mzozo na wafanyakazi wenzake wa Shirika la UNDP.