Baraza la Usalama la UN kuiondolea vikwazo Eritrea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49266-baraza_la_usalama_la_un_kuiondolea_vikwazo_eritrea
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kuiondolea vikwazo Eritrea ndani ya siku chache zijazo, ilivyowekewa mwaka 2009 kwa tuhuma za kuliunga mkono kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab la nchi jirani ya Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 04, 2018 04:34 UTC
  • Baraza la Usalama la UN kuiondolea vikwazo Eritrea

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kuiondolea vikwazo Eritrea ndani ya siku chache zijazo, ilivyowekewa mwaka 2009 kwa tuhuma za kuliunga mkono kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab la nchi jirani ya Somalia.

Rasimu ya azimio hilo la kuiondolea nchi hiyo ya Pembe ya Afrika vikwazo iliyotayarishwa na Uingereza inatazamiwa kupigiwa kura Novemba 14 na nchi wanachama wa Baraza la Usalama la UN.

Uingereza na Ufaransa hata hivyo zinasisitiza kuwa, sharti Eritrea ionyeshe hatua ilizopiga katika kuheshimiwa haki za binadamu nchi humo, kabla ya vikwazo hivyo kuondolewa kikamilifu. Marekani ambayo imekuwa ikipinga kuondolewa vikwazo taifa hilo la Pembe ya Afrika hivi karibuni ilighairi msimamo wake huo.

Ethiopia hivi karibuni iliomba kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Eritrea baada ya nchi hizo mbili kusaini Azimio la Amani na Urafiki tarehe 9 Julai mwaka huu na kurejesha uhusiano wa nchi mbili kwenye hali ya kawaida.

Rais wa Eritrea, Isais Afwerki (kulia) na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abey Ahmed

Ethiopia pia imesema imeazimia kuzisaidia Eritrea na Djibouti kutatua mgogoro wao wa mpaka, ili uhusiano wa nchi hizo pia urudi katika hali ya kawaida.

Eritrea imekuwa ikisisitiza kuwa vikwazo hivyo vya miaka tisa ni vya kidhalimu na havikuwa na msingi wa kisheria au haki na imetaka ilipwe fidia kutokana na hasara ilizopata baada ya kuwekewa vikwazo.