Mchungaji Msigwa: Wafanyabiashara wakubwa nchini Tanzania hawana amani wala uhuru      
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49345-mchungaji_msigwa_wafanyabiashara_wakubwa_nchini_tanzania_hawana_amani_wala_uhuru
Mbunge wa Iringa Mjini nchini Tanzania kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa amesema kuwa, wafanyabiashara wakubwa nchini humo hawana raha wala uhuru wa kufanya biashara ndani ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2018 04:25 UTC
  • Mchungaji Msigwa: Wafanyabiashara wakubwa nchini Tanzania hawana amani wala uhuru       

Mbunge wa Iringa Mjini nchini Tanzania kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa amesema kuwa, wafanyabiashara wakubwa nchini humo hawana raha wala uhuru wa kufanya biashara ndani ya nchi hiyo.

Msigwa ameyasema hayo bungeni wakati akichangia mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2019/20 ambapo sambamba na kuzungumzia tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini humo hivi karibuni, Mohamemd Dewji ‘Mo’ amehoji ni kwa nini mfanyabiashara huyo hakupewa nafasi ya kusema alikuwa wapi wakati alipotekwa nyara na watu wasiojulikana. “Je, watu wetu wako salama? Matajiri hawana raha, juzi kafichwa akatekwa mfanyabiashara bilionea (Mo). Nani atakuwa na raha? Hakupewa hata nafasi ya kusema alikuwa wapi.” Alisema Msigwa.

Mohammed Dewji, bilionea kijana aliyetekwa nyara hivi karibuni

Aidha mbunge huyo wa Iringa Mjini amesema hadi leo hakuna taarifa yoyote inayoonyesha ni nani aliyemteka na pia alikuwa wapi, huku akihoji kwa sasa diplomasia ya Tanzania ikoje?. Katika sehemu nyingine amezungumzia uhusiano wa nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi za Magharibi kwa kusema: “Kama leo Balozi wa Ulaya anaitwa nchini kwake kujadili ilivyo hali ya Tanzania ilivyo, basi serikali ijiulize mahusiano yake na mataifa mengine yakoje? Wafanyabiashara wanafunga virago wanaondoka kwa sababu wanaona hawako sawa. Kadhalika Msigwa amesema kwamba, Tanzania inahitaji katiba ambayo itawaunganisha Watanzania wote.