Nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika kushirikiana mipaka
Nchi nane za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika zimeazimia kuanzisha shirika la kiufundi la ushirikiano mipakani litakalowezesha utekelezaji wa masuala 22 kwa lengo la kuboresha ushirika na kuimarisha utendaji wa operesheni za mipakani.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji , IOM, mipaka ya eneo hilo ni miongoni mwa mipaka iliyo na shughuli nyingi kwa sababu ndio njia muhimu ya wahamiaji kutoka kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika lakini pia kuelekea sehemu zingine duniani ikiwemo Ulaya na nchi za Ghuba ya Uajemi.
Shirika hilo linasema kuimarisha ushirikiano mipakani miongoni mwa nchi hizi ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia na Djibouti si kazi rahisi lakini kuna matumaini baada ya warsha iliyofanyika mjini Nairobi Kenya na kujumuisha pande zote.
Warsha ya kwanza ya nchi hizo imefanyika Nairobi, Kenya ambapo mikataba muhimu ilifikiwa na kutiwa sahihi na wakurugenzi na maafisa wa uhamiaji kutoka nchi hizo nane chini ya kauli mbiu “mpango wa udhibiti bora wa uhamiaji” (BMM).
Kwa mara ya kwanza miongoni mwa mikataba iliyowekwa saini ni baina ya Ethiopia na Sudan Kusini kufanya doria ya pamoja na kushirikiana kufungua kituo kipya cha uhamiaji baina ya nchi hizo mbili. Sudan na Sudan Kusini zilitia saini kufanya kazi pamoja kufungua vituo vinne vya ukaguzi mipakani mwao kikiwemo kituo kikubwa kimoja cha pamoja.

Uganda na Sudan Kusini zimeafikiana kuanzisha na kutekeleza ushirika wa doria mipakani na kuzindua kamati za udhibiti wa mipaka .
Kwa upande wa Tanzania, Somalia na Kenya zimekubaliana kutekeleza mpango wa kamati za pamoja za udhibiti mipakani na kuwa na shirika la pamoja, vilevile kufanya doria mipakani.
Nazo Ethiopia, Kenya na Tanzania zimeafikiana kuongeza ushirikiano na utekelezaji wa masuala mazuri muhimu katika kupambana na usafirishaji haramu, na kufanya doria za pamoja mipakani.