UNHCR: Zaidi ya Wacameroon 30,000 wamekimbilia nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49419-unhcr_zaidi_ya_wacameroon_30_000_wamekimbilia_nchini_nigeria
Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amesema kuwa, idadi ya raia wa Cameroon waliokimbilia nchini Nigeria kukwepa machafuko katika nchi yao imeongezeka na kupindukia 30,000.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Nov 10, 2018 10:43 UTC
  • UNHCR: Zaidi ya Wacameroon 30,000 wamekimbilia nchini Nigeria

Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amesema kuwa, idadi ya raia wa Cameroon waliokimbilia nchini Nigeria kukwepa machafuko katika nchi yao imeongezeka na kupindukia 30,000.

Babar Baloch amesema katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Geneva Uswsi kwamba, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita takribani raia 600 kutoka Cameroon wameingia katika maeneo maalumu ya kuhifadhia wakimbizi nchini Nigeria.

Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa amesema kuwa, wakimbizi ambao hivi karibuni waliingia katika kambi za wakimbizi nchini Nigeria ni wenyeji wa miji ya Eyumojock na Akwaya nchini Cameroon.

Aidha Babar Baloch amesema kkuwa, aghalabu ya wakimbizi hao wanasema kuwa, vitendo vya utumiaji mabavu katika maeneo yao vinazidi kuongezeka na kwamba, wamekuwa wakitakiwa kuyahama makazi yao.

Maandamano ya raia wa Cameroon wanaozungumza Kiingereza ambao wanataka kujitenga na serikali kuu

Takwimu zinaonyesha kuuwa, kila wakimbizi watano wanaojiandikisha katika kambi za wakimbizi nchini Nigeria, wanne kati yao ni wanawake na watoto wadogo.

Machafuko yameongezeka sana katika miezi ya hivi karibuni katika maeneo yenye wazungumzaji wengi wa Kiingereza huko nchini Cameroon.

Wazungumzaji wa Kiingereza wanaunda karibu asilimia 20 ya wakazi wote milioni 20 wa nchi ya Cameroon iliyoko magharibi mwa Afrika. 

Wazungumzaji hao wa Kiingereza wanalalamika kuwa wananyanyaswa na kutengwa na serikali kuu na wananyimwa haki zao kama raia wa Cameroon hivyo wanaona ni vyema wapiganie kujitenga.