Mbowe na Mbunge Ester Matiko wapelekwa mahabusu kwa muda usiojulikana nchini Tanzania
Mahakama Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Tanzania, imewafutia dhamana Mwenyekiti wa chama cha Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Matiko kwa madai ya ukiukaji wa masharti ya dhamana, na kuanzia sasa watakuwa rumande hadi hapo kesi yao itakapomalizika.
Uamuzi huo umetokana na maombi yaliyotolewa na upande wa mashtaka ambao umedai kwamba, washtakiwa hao wamekiuka masharti ya dhamana kwa kusafiri nje ya nchi bila kibali cha mahakama na kushindwa kuripoti katika kituo cha polisi cha wilaya ya Ilala. Aidha upande wa mashtaka umechukua hatua hiyo kutokana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kushindwa kufika mahakamani hapo tarehe Mosi na tarehe nane, huku Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Matiko naye akishindwa kufika mahakamani hapo tarehe nane ya mwezi huu kwa ajili ya kusikiliza kesi inayowakabili.
Hii ni katika hali ambayo wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala, ameieleza mahakama hiyo ya Kisutu kwamba wao kama watetezi wa washtakiwa wataukatia rufaa uamuzi huo alioutaja kuwa si sahihi. Mbowe, Matiko na wenzao saba katika kambi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA nchini Tanzania wanakabiliwa na kesi ya jinai yenye jumla ya mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi na uchochezi wa uasi. Wakati huo huo Mbowe amewataka wanachama na viongozi wa chama chake kuwa imara na kutoogopa huku akisisitiza kwamba, kesho ni nzuri kuliko jana. "Naomba muwe stable (imara) msiogope. Kesho ni nzuri kuliko jana." Amesema Mbowe. Kiongozi huyo wa upinzani ameyasema hayo wakati polisi walipotaka kumuondoa kizimbani ambapo kwanza aliwataka askari hao kuzungumza na watu wake. Mbali na Mbowe, viongozi wengine wa CHADEMA wanaotuhumiwa katika faili hilo ni pamoja na DK Vicent Mashinji, Katibu Mkuu, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda, John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini na Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, jijini Dar es Salaam.