Nduli wa mauaji ya Waislamu CAR apandishwa kizimbani ICC
(last modified Sat, 24 Nov 2018 02:46:54 GMT )
Nov 24, 2018 02:46 UTC
  • Nduli wa mauaji ya Waislamu CAR apandishwa kizimbani ICC

Alfred Yakatom, ambaye wakati fulani alijulikana kwa jina la Rambo kutokana na kufanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC akikabiliwa na mashtaka 14 ya jinai za kivita na jinai dhidi ya ubinadamu.

Wakili wa mtuhumiwa huyo ambaye ni maarufu kwa kutesa na kufanya mauaji ya kutisha dhidi ya Waisamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kuwa, mteja wake huyo aliteswa kabla ya kupelekwa Uholanzi kusikiliza kesi yake mjini The Hague, ingawa hata hivyo hakutoa ushahidi wa maana kuhusu madai yake hayo.

Nduli huyo wa mauaji ya Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati alitiwa mbaroni na maafisa wa serikali ya nchi hiyo tarehe 29 Oktoba mwaka huu kabla ya kukabidhiwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Nduli Alfred Yekatom mbele ya mahakama ya kimataifa ya ICC (Chanzo: aljazeera.com)

 

Katika siku yake ya kwanza ya kupandishwa kizimbani kwenye mahakama hiyo ya ICC, Alfred Yekatom alithibitisha jina na umri wake kama ambavyo amesema pia kuwa amesoma na kuelewa mashtaka yake. Kikao cha kutajwa kesi hiyo kilichukua muda wa dakika 35 hiyo jana Ijumaa. 

Miongoni mwa mashtaka 14 yanayomkabili nduli huyo wa mauaji ya Waislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ni jinai dhidi ya ubinadamu inayojumuisha mauaji, kukata viungo vya watu, kutesa, kuamiliana vibaya na wahanga na kuingiza watoto wadogo katika masuala ya kijeshi kupitia genge lake la Kikristo la Anti Balaka. 

Genge hilo la Kikristo linatuhumiwa kuwashambulia wananchi wa kawaida Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati baina ya mwezi Disemba 2013 na Agosti 2014.

Tags