Sisitizo la Waziri Mkuu wa Uhispania juu ya jibu kali la jamii ya kimataifa kwa jinai za utawala wa Israel
Waziri Mkuu wa Uhispania ametaja oparesheni ya kijeshi ya utawala habithi wa Israeli huko Lebanon kuwa "uvamizi" na kusisitiza kwamba jamii ya kimataifa inapasa kuchukua hatua kuhusu suala hilo.
Akizungumza kwenye bunge la Uhispania, Pedro Sanchez, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, amesema: "Ni dhahiri kwamba Israel imevamia na kukalia kwa mabavu nchi huru kama Lebanon, hivyo jamii ya kimataifa haiwezi kunyamaza kimya."
Waziri Mkuu wa Uhispania ameongeza kwa kusema: "Sisi tunalaani hali hii katika Ukanda wa Gaza na Lebanon."
Vile vile amekosoa vikali hatua za utawala haramu wa Israel za kutoheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu huko Ukanda wa Gaza, na kusema hatua hizo zimeikasirisha sana Uhispania.
Pedro Sanchez ni miongoni mwa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, ambaye amekuwa akiukosoa vikali utawala wa Kizayuni kutokana na jinai zake dhidi ya watu wa Palestina.
Yapata miezi mitano iliyopita Uhispania, chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Pedro Sanchez, iliitambua rasmi Palestina kuwa nchi huru.
Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza ilitangaza Jumatano ya wiki hii katika takwimu zake za karibuni zaidi kwamba, zaidi ya Wapalestina 42,000 wameuawa shahidi kutokana na vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa ukanda huo.