Miili ya wahajiri 15 yapatikana ndani ya boti katika bahari ya Mediterania
Maiti za wahajiri 15 wa Kiafrika zimepatikana na jeshi la majini la Morocco, zikiwa ndani ya boti iliyokuwa ikielea katika bahari ya Mediterania.
Taarifa ya jeshi hilo imesema kuwa, wapiga mbizi wa Gadi ya Pwani ya Morocco waliipata miili hiyo ndani ya boti iliyoonekana kuwa injini yake ilifeli siku chache zilizopita, ikiwa njiani kuelekea nchini Uhispania, na kwamba wamefanikiwa kuokoa makumi ya wahajiri wengine.
Habari zaidi zinasema kuwa, wanawake wanane ni miongoni mwa wahajiri 53 waliokolewa kwenye operesheni hiyo ya jana Jumamosi, na wamepekwa katika mji bandari wa Nador.
Inaarifiwa kuwa, wahajiri hao ni raia wa nchi za eneo la chini ya jangwa la Sahara barani Afrika, ambao walikuwa katika safari hiyo hatarishi kwenda Ulaya kutafuta maisha.
Ijumaa iliyopita, jeshi la majini la Morocco liliwaokoa wahamiaji wengine 289 waliokuwa kwenye boti dhaifu wakielekea Uhispania, katika moja ya safari ambazo zimeua wahajiri 630 tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.
Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya wahajiri 93 kujifungia kwenye shehena iliyoko ndani ya meli moja katika mji bandari wa Misrata kwa muda wa siku tano sasa baada ya kuokolewa, wakisisitiza kuwa Libya ni nchi hatari sana kwao.
Itakumbukwa kuwa, wahajiri wanane wakiwemo watoto sita walipoteza maisha baada ya kuishiwa na hewa wakiwa ndani ya kasha la kusafirishia mizigo katika mji wa Zuwara ulioko katika pwani ya magharibi mwa Libya mwezi Julai mwaka huu.