Wahajiri 113 waokoloewa katika fukwe za magharibi mwa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49786-wahajiri_113_waokoloewa_katika_fukwe_za_magharibi_mwa_libya
Jeshi la Majini la Libya limetangaza habari ya kuokoa wahajiri haramu 113 katika fukwe za magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 26, 2018 23:11 UTC
  • Wahajiri 113 waokoloewa katika fukwe za magharibi mwa Libya

Jeshi la Majini la Libya limetangaza habari ya kuokoa wahajiri haramu 113 katika fukwe za magharibi mwa nchi hiyo.

Jeshi hilo limetangaza kuwa, gadi ya fukwe za Libya kwa kushirikiana na meli moja ya kuchimba gesi ya Libya wamefanikiwa kuwaokoa wahajiri hao ambapo walikuwemo pia wanawake na watoto wadogo kutoka nchi tofauti za Afrika, katika umbali wa kilomita 75 kutoka kwenye fukwe za mji mkuu Tripoli. 

Taarifa ya jeshi hilo imeongeza kuwa, baada ya kuokolewa, wahajiri hao wamepelekwa kwenye kituo cha kuhifadhia wahajiri cha mji wa Zawiya ulioko umbali wa kilomita 45 magharibi mwa Tripoli.

Wahajiri haramu Libya

 

Kutokana na kukosekana usalama na utulivu wa kisiasa baada ya matukio ya mwaka 2011 na uvamizi wa kijeshi wa Marekani na NATO nchini humo, hivi sasa Libya imebadilika kuwa kituo kikuu cha kusafirishia wahajiri haramu kutoka nchi mbali mbali za Afrika na Mashariki ya Kati.

Magenge ya magendo ya binadamu yanatumia fursa hiyo kuingiza nchini Libya makumi ya maelfu ya wahajiri haramu kila mwaka. Wahajiri hao wanatozwa fedha nyingi sana na wako tayari kupoteza roho zao na kila walicho nacho kwa ajili ya kufika barani Ulaya.

Asilimia kubwa ya wahajiri hao wenye tamaa kupindukia huwa hawafiki wanakokwenda, bali huishia mikononi mwa magenge ya kigaidi na ya magendo ya binadamu, au kuzama baharini na kupigwa mnada masokoni na kuuzwa kama watumwa.