Nchi za Afrika zalenga kurahisisha biashara ya kikanda na kimataifa
Nchi za Afrika ambazo zinalenga kupunguza gharama, muda na urasimu wa kufanya biashara ya kikanda na kimataifa zinakutana huko Addis Ababa, Ethiopia, katika warsha ya kwanza kabisa ya Afrika kwa ajili ya kuunda kamati za kuwezesha biashara.
Warsha hiyo ya aina yake ya siku tatu ilianza jana na imeandaliwa na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Biashara na Maendeleo, UNCTAD na wadau wa sekta hiyo. Warsha hiyo inafanyika wakati huu ambapo bara la Afrika limeimarisha juhudi za kurahisisha ufanyaji biashara kufuatia makubaliano ya biashara ya Shirika la Biashara Duniani, WTO na wakati ikisubiriwa kutekelezwa makubaliano ya eneo huru la biashara barani Afrika, AfCFTA, yaliyotiwa saini mwezi Machi 2018.

Akizungumzia warsha hiyo, Katibu Mtendaji wa UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi amesema, WTO inakadiria gharama ya kufanya biashara katika mataifa yanayoendelea kuwa ni sawa na asilimia 219 ya ushuru kwa biashara ya kimataifa, hali ambayo inaliathiri vibaya bara hilo.
Kwa mujibu wa UNCTAD lengo la warsha hiyo ni kuhakikisha kila nchi inaweka kamati ya taifa ya kusimamia biashara ikijumuisha sekta binafsi na ya umma kwa ajili ya kusimamia biashara nyumbani na kufuatilia makubaliano ya warsha.