Uganda iliisadia Sudan Kusini kukiuka vikwazo vya silaha vya EU
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49851-uganda_iliisadia_sudan_kusini_kukiuka_vikwazo_vya_silaha_vya_eu
Kundi moja la kudhibiti silaha leo limeeleza kuwa Uganda ilisaidia kuingiza nchini Sudan Kusini silaha na zana za kijeshi za Ulaya wakati wa vita vya ndani nchini humo na hivyo kukiuka vikwazo vya silaha vya Umoja wa Ulaya dhidi ya nchi hiyo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Nov 29, 2018 10:05 UTC
  • Uganda iliisadia Sudan Kusini kukiuka vikwazo vya silaha vya EU

Kundi moja la kudhibiti silaha leo limeeleza kuwa Uganda ilisaidia kuingiza nchini Sudan Kusini silaha na zana za kijeshi za Ulaya wakati wa vita vya ndani nchini humo na hivyo kukiuka vikwazo vya silaha vya Umoja wa Ulaya dhidi ya nchi hiyo.

Kundi hilo kwa jina la Conflict Armament Research lenye makao yake nchini Uingereza limesema kuwa Sudan Kusini  ilitoa dhamana kwa serikali  ya Uganda ya kuinunulia silaha na zana za kijeshi kutoka Bulgaria, Romania na Slovakia. Silaha hizo ziliingizwa nchini Uganda mwaka 2014 na 2015 baadaye zilisafirishwa hadi katika nchi jirani ya Sudan Kusini. Hayo ni kwa mujibu wa utafiti wa miaka minne uliofanywa na kundi hilo la kudhibiti silaha. 

Msemaji wa jeshi la Uganda amejizuia kutoa jibu lolote kuhusu tuhuma hizo zilizoelekezwa kwa serikali ya nchi hiyo hadi hapo atakaposoma ripoti ya kundi hilo. Ripoti hiyo pia imeeleza namna maafisa wa kijeshi wa ngazi ya juu wa Sudan Kusini walivyohusika katika mchakato mzima kuanzia mwanzo hadi mwisho. James Bevan Mkuu wa Kundi hilo la Kudhibiti Silaha (CAR) amesema kuwa serikali ya Uganda bila kuficha ilitoa silaha na wanajeshi kwa Sudan Kusini ikiwa ni katika kuliunga mkono jeshi la nchi hiyo katika vita vilivyoanza nchini humo mwaka 2013.

James Bevan, Mkuu wa Kundi la Kudhibiti Silaha lenye makao yake nchini Uingereza