Sudan Kusini yakanusha kukiuka marufuku ya usafirishaji silaha
Sudan Kusini imekanusha tuhuma kuwa nchi jirani yake Uganda inaisaida kupata silaha za Ulaya licha ya vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya.
Katika taarifa , serikali ya Sudan Kusini imesema hivi sasa inafuatilia kuwekeza katika makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni wala sio vita. Ripoti iliyotolewa na kundi moja lenye makao makuu mjini London imesema serikali ya Uganda ilinunua silaha na risasi kutoka kwa nchi tatu za Umoja wa Ulaya na kuzisafirisha kwa jeshi la Sudan Kusini kati ya mwaka 2014 hadi mwaka 2015.
Ripoti hiyo imesema Sudan Kusini ilitoa dhamana kwa serikali ya Uganda ya kuinunulia silaha na zana za kijeshi kutoka Bulgaria, Romania na Slovakia. Uchunguzi wa shirika la Utafiti wa Silaha Vitani - Conflict Armament Research - CAR, umebaini kuwa nchi jirani, hasa Uganda, huchangia kuisaidia Sudan Kusini kukwepa vikwazo vya silaha.
Msemaji wa serikali ya Sudan Kusini Michael Makuei ameitaja ripoti hiyo kuwa bandia huku akisisitiza kuwa wakuu wa Juba sasa wanafuatilia amani. Amesema walioandika ripoti hiyo wanapinga amani na wanalenga kuvuruga mapatano ya sasa ya amani.
Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kupelekea mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.
Hivi karibuni pande hasimu zilifikia mapatano ya amani na inatarajiwa kuwa utulivu utarejea nchini humo.