Kenya yaomba msaada wa IAEA kutumia teknolojia ya nyuklia kutibu saratani
(last modified Fri, 30 Nov 2018 07:25:38 GMT )
Nov 30, 2018 07:25 UTC
  • Kenya yaomba msaada wa IAEA kutumia teknolojia ya nyuklia kutibu saratani

Kenya imeomba msaada wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuisaidia kuimarisha matibabu ya saratani katika hospitali mbili kubwa nchini humo na pia kueneza huduma hizo za matibabu katika miji mingine mitatu.

Mwito huo umetolewa na Waziri wa Nishati Kenya Charles Keter alipohutubia jana kikao cha mawaziri cha IAEA mjini Vienna Austria. Keter pia amesema Kenya iko mbioni kuunda kiwanda cha kuzalisha nishati ya nyuklia. Ameongeza kuwa serikali ya Kenya ina mpango wa kufungua vituo vipya vya matibabu ya saratani kwa kutumia teknolojia ya nyuklia katika Hospitali Kuu ya Pwani mjini Mombasa, Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga mjini Kisumu na Hospitali Kuu ya Nyeri eneo la Kati. Ameishukuru IAEA kwa mchango wake mkubwa katika kuanzishwa vituo vya matibabu ya saratani kwenye Hospitali Kuu ya Kenyatta mjini Nairobi na Hospitali ya Eldoret.

Keter amesema, ugonjwa wa saratani unaongezeka kwa kasi Kenya na wagonjwa wengi hulazimika kwenda India kupata matibabu. Amesema iwapo Kenya itapata suhula bora za matibabu, itaweza kuzihudumia pia nchi zote za eneo la mashariki mwa Afrika.

Kwa upande wake, Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA amesema, Kenya ni kati ya vituo vya wakala huo duniani na ameahidi kusaidia ujenzi wa vituo vya kutibu kensa au saratani katika miji ya Mombasa, Nyeri na Kisumu.