UN: Nchi za Afrika zinapora bajeti inayotengwa kwa ajili ya wakimbizi
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, baadhi ya nchi za Kiafrika zinapora na kutumia vibaya fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi barani humo.
Ripoti iliyotolewa na Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, miongoni mwa mifano ya wazi na mashuhuri zaidi ya uporaji wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya Shirika la Wakimbizi la Umoja huo barani Afrika ni dola laki tatu na 20 elfu za bajeti ya wakimbizi zilizotumiwa kujenga egesho la magari la Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uganda.
Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa imesisitiza kuwa, Uganda na Sudan Kusini pekee zimetumia vibaya zaidi ya dola milioni 11 za bajeti ya operesheni kubwa zaidi ya kuwasaidia wakimbizi barani Afrika na kwamba, fedha hizo zimetumiwa kwa ajili ya wakimbizi mazimwi na wasiokuwepo.
Ripoti hiyo ya Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani ya Umoja wa Mataifa imesema katika kesi nyingine idara ya wakimbizi ya UN kwa ajili ya Afrika imetoa dola milioni 7.9 ya bajeti yake kwa kampuni moja kwa ajili ya kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 1200 ambayo kimsingi haina utaalamu katika sekta.