Burundi yatoa waranti ya kukamatwa rais wa zamani wa nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49881-burundi_yatoa_waranti_ya_kukamatwa_rais_wa_zamani_wa_nchi_hiyo
Serikali ya Burundi imetoa waranti ya kimataifa ya kutiwa mbaroni rais wa zamani wa nchi hiyo, Pierre Buyoya kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kiongozi wa kwanza wa jamii ya Wahutu kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia, Melchior Ndadaye.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Dec 01, 2018 04:36 UTC
  • Burundi yatoa waranti ya kukamatwa rais wa zamani wa nchi hiyo

Serikali ya Burundi imetoa waranti ya kimataifa ya kutiwa mbaroni rais wa zamani wa nchi hiyo, Pierre Buyoya kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kiongozi wa kwanza wa jamii ya Wahutu kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia, Melchior Ndadaye.

Mwanasheria Mkuu wa Burundi, Sylvestre Nyandwi alisema Ijumaa ya jana kuwa, Buyoya pamoja na shakshia wengine 16 waliokuwa viongozi wa ngazi za juu serikalini enzi hizo walihusika katika kuratibu mauaji ya Ndayaye mwaka 1993.

Amesema ripoti ya jopo la uchunguzi imewapata na hatia viongozi hao, na kwamba vyombo vya mahakama vya Burundi vinaandaa mazingira ya kuwakamata na kuwashitaki.

Miongoni mwa watu hao wanaotuhumiwa kuhusika na jinai hiyo ni maafisa 11 wa zamani wa Wizara ya Ulinzi na raia watano waliokuwa wapambe wa karibu wa Buyoya.

Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya 

Mwanasheria Mkuu wa Burundi amesema serikali ya Bujumbura inatoa mwito kwa nchi ambazo washukiwa hao wanaishi kuwakamata na kuwakabidhi kwa serikali ya Burundi.

Buyoya, Mtutsi ambaye aliingia madarakani kwa msaada wa jeshi hapo mwaka 1987, kwa sasa ni Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika nchini Mali.

Kuuawa kwa Ndadaye mwaka 1993, kulipelekea kutokea mapigano baina ya Wahutu na Watutsi nchini Burundi, ambapo watu zaidi ya laki tatu waliuawa.