Wakimbizi raia wa Ivory Coast watakiwa kurejea nchini kwao
Serikali ya Ivory Coast imewataka raia wa nchi hiyo ambao wamekimbilia katika nchi jirani na kuomba hifadhi ya ukimbizi kurejea nchini kwao.
Mariatou Kone, Waziri wa Mshikamano na Mfungano wa Kijamii wa Ivory Coast amewataka wanajeshi na raia wa nchi hiyo ambao kuanzia mwaka 2011 walikimbilia jirani na kuomba hifadhi ya ukimbizi kurejea nchini kwao.
Waziri huyo amesema kuwa, ili Rais Alassane Ouattara wa nchi hiyo aweze kutekeleza vyema mipango ya ujenzi na ukarabati wa nchi anawahitajia raia wote wa nchi hiyo.
Waziri wa Mshikamano na Mfungano wa Kijamii wa Ivory Coast amebainisha kwamba, viongozi wa nchi hiyo watafanya kila wawezalo kuhuisha uchumi wa nchi na hali ya kijamii ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Tangu alipoingia madarakani Rais Alassane Ouattara wa Côte d’Ivoire amekuwa akikabiliwa na upinzani mkubwa nchini humo. Wafuasi wa utawala uliopita wamekuwa wakitaka kuachiliwa huru rais wa zamani wa nchi hiyo Laurent Gbagbo, ambaye anaendelea kushikiliwa na Mahakama ya Makosa ya Jinai ya Kimataifa ICC.