Libya yatangaza tarehe ya kufanyika kura ya maoni ya katiba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50012-libya_yatangaza_tarehe_ya_kufanyika_kura_ya_maoni_ya_katiba
Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Libya ametangaza tarehe ya kufanyika kura ya maoni kuhusu katiba ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 07, 2018 04:42 UTC
  • Libya yatangaza tarehe ya kufanyika kura ya maoni ya katiba

Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Libya ametangaza tarehe ya kufanyika kura ya maoni kuhusu katiba ya nchi hiyo.

Emad al Sayeh amewaambia waandishi wa habari mjini Tripoli kwamba, mchakato wa kura ya maoni kuhusu katiba mpya ya nchi hiyo utaanza katika nusu ya kwanza ya mwezi Februari mwaka ujao wa 2019 na zoezi rasmi la upigaji kura litafanyika kabla ya kumalizika mwezi Februari. 

Tangazo hilo la Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Libya ni ishara mafanikio katika jitihada za kurejesha umoja na utulivu nchini humo baada ya miaka kadhaa ya machafuko. 

Afisa huyo wa Libya amesisitiza kuwa, kufanikiwa kura hiyo ya maoni kunategemea masuala manne ambayo ni mapatano ya kisiasa, kuwepo sheria ya kura ya maoni, kulindwa usalama wa makao makuu ya Tume Kuu ya Uchaguzi na kudhamini usalama wakati wa zoezi la upigaji kura. 

Libya inasumbuliwa na mapigano ya ndani.

Libya ilitumbukia katika mivutano na mapigano ya ndani mwaka 2011 kutokana na uingiliaji kati wa muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi (NATO) na Marekani. Hitilafu kubwa baina ya makundi ya ndani zimewafanya Walibya washindwe kuasisi serikali moja na sasa nchi hiyo inatawaliwa na serikali mbili tofauti.