Wanajeshi wawili wauawa katika shambulio la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50071-wanajeshi_wawili_wauawa_katika_shambulio_la_boko_haram_kaskazini_mashariki_mwa_nigeria
Maafisa usalama wa Nigeria wametangaza kuwa, shambulio lililofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram dhidi ya kambi moja ya jeshi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo limepelekea wanajeshi wawili kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 10, 2018 03:19 UTC
  • Wanajeshi wawili wauawa katika shambulio la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria

Maafisa usalama wa Nigeria wametangaza kuwa, shambulio lililofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram dhidi ya kambi moja ya jeshi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo limepelekea wanajeshi wawili kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Taarifa ya maafisa usalama wa Nigeria iimesema kuwa, shambulio hilo la wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram limefanywa katika jimbo la Borno na kwamba, baadhi ya wanajeshi waliojeruhiwa katika shambulio hilo hali zao ni mbaya.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, wanamgambo wa Boko Haram wameshadidisha mashambulio yao katika siku za hivi karibuni katika maeneo mbalimbali ya kaskazini mashariki mwa Nigeria hususan dhidi ya vituo na kambi za jeshi.

Hivi sasa kundi hilo limekuwa likiendesha vitendo vya kigaidi katika nchi za Cameroon, Chad, Niger na Nigeria, na mpaka sasa limeshapelekea watu zaidi ya milioni 2.4 kwenye eneo za Ziwa Chad wayakimbie makazi yao.

Rais Muhamadu Buhari, serikali yake inakosolewa kwa kushindwa kulisambaratisha kundi la Boko Haram

Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009.

Boko Haram ni kundi linalofuata itikadi za Kiwahhabi na limeitumbukiza Nigeria katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha mizozo ya kidini na kikabila katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Licha ya serikali ya Nigeria kutangaza mwishoni mwa mwaka 2015 kuwa kundi la Boko Haram limesambaratishwa kwa kiasi kikubwa, lakini kundi hilo lingali lina uwezo wa kufanya mashambulizi katika mji wa Maiduguri, maeneo ya karibu yake na katika maeneo mengi ya kaskazini mashariki mwa Nigeria.