Makumi ya watu wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Ethiopia
(last modified Sat, 15 Dec 2018 07:18:40 GMT )
Dec 15, 2018 07:18 UTC
  • Makumi ya watu wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Ethiopia

Watu wasiopungua 21 wameuawa katika mapigano ya kikabila kusini mwa Ethiopia.

Radio ya FANA ya serikali ya Ethiopia imeripoti habari hiyo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, mapigano ya kikabila ya siku mbili yametokea karibu na mji wa Moyale, mpakani mwa nchi hiyo na Kenya.

Watu wa kabila la Oromia

Habari zaidi zinasema kuwa, watu wengine 60 wamejeruhiwa katika mapigano hayo, baina ya makabila mawili ya eneo hilo, ambalo Waoromo wanadai ni lao.

Hivi karibuni pia, watu 23 waliuawa katika machafuko yaliyozuka jirani na mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa, baada ya wafuasi wa kundi la zamani la waasi la Harakati ya Ukombozi wa Oromo (OLF) ambao wengi wao wanatoka kabila la Oromo, kuingia mjini Addis Ababa wakipeperusha bendera ya OLF, na kupambana na wakazi wa mji huo.

Aidha Agosti mwaka huu, watu wasiopungua 40 waliuawa mashariki mwa Ethiopia katika wimbi la machafuko yaliyochochewa na migawanyiko ya kikabila, katika eneo la mpaka wa Somalia na mikoa ya Oromiya. 

Machafuko ya kikabila yalienea katika mkoa wa Oromiya tangu yalipofanyika maandamano mwaka 2015 ya kudai kupatiwa haki ya kumiliki ardhi.