Nchi za Afrika zahitaji nafasi milioni 20 za ajira kwa mwaka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50244-nchi_za_afrika_zahitaji_nafasi_milioni_20_za_ajira_kwa_mwaka
Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF Bi. Christine Lagarde amesema nchi za Afrika za kusini mwa jangwa la Sahara zinapaswa kuongeza ajira milioni 20 kwa mwaka kutokana na ongezeko la kasi la idadi ya watu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 18, 2018 03:18 UTC
  • Nchi za Afrika zahitaji nafasi milioni 20 za ajira kwa mwaka

Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF Bi. Christine Lagarde amesema nchi za Afrika za kusini mwa jangwa la Sahara zinapaswa kuongeza ajira milioni 20 kwa mwaka kutokana na ongezeko la kasi la idadi ya watu.

Bibi Lagarde ambaye yuko ziarani nchini Ghana, aliyasema hayo jana Jumatatu mjini Accra kwenye ufunguzi wa mkutano wa IMF kuhusu mustakabali wa ajira katika nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.

Amesema idadi ya watu katika nchi hizo itaongezeka na kufikia bilioni 1.7 ifikapo mwaka 2040 kutoka bilioni 1 ya sasa, na wakati huohuo kasi ya ongezeko la nguvukazi itakuwa maradufu kuliko ile ya mwongo uliopita.

Kiwanda cha magari nchini Kenya

Nchi hizo zitahitaji kuongeza ajira milioni 20 kwa mwaka kuendana na ongezeko la nguvu kazi. Amesema zikifanikiwa kufanya hivyo, bara la Afrika litakuwa na ongezeko la kasi kwa muda mrefu, ambalo ni moja kati ya faida zinazoletwa na ongezeko la watu.

Lagarde aidha amewapongeza viongozi wa Afrika kwa kuafikia Mapatano ya Biashara Huru na kusema hiyo ni hatua ya kwanza chanya katika kuunda soko la pamoja la Afrika.