Watu kumi wafariki dunia katika mlipuko wa bomu nchini Ethiopia
Kwa akali watu 10 wamefariki dunia nchini Ethiopia na mwingine mmoja kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko mkubwa wa bomu la kutegwa kando ya barabara moja magharibi mwa nchi hiyo.
Vyombo vya usalama vya Ethiopia vimetangaza kuwa, mlipuko huo uliolilenga basi dogo la abiria ulitokea jana katika barabara kuu iliyoko baina ya jimbo la Oromia na Benishangul-Gumuz.
Kamishna Mkuu wa polisi wa mji wa Benishangul- Gumuz amelilaumu kundi la Oromo Liberation Front (OLF) ambalo hivi karibuni lilitiliana saini makubaliano ya amani na serikali ya Addis Ababa inayoongozwa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed.
Hivi karibuni pia watu 23 waliuawa katika machafuko yaliyozuka jirani na mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa, baada ya wafuasi wa kundi la zamani la waasi la Harakati ya Ukombozi wa Oromo (OLF) ambao wengi wao wanatoka katika kabila la Oromo, kuingia mjini Addis Ababa wakipeperusha bendera ya OLF na kupambana na wakazi wa mji huo.

Itakumbukwa kuwa, Agosti mwaka huu, watu wasiopungua 40 waliuawa mashariki mwa Ethiopia katika wimbi la machafuko yaliyochochewa na migawanyiko ya kikabila.
Machafuko ya kikabila yalienea katika mkoa wa Oromia tangu yalipofanyika maandamano mwaka 2015 ya kudai kupatiwa haki ya kumiliki ardhi.
Mwezi uliopita kuligunduliwa kaburi la umati lenye miili 200 katika eneo lililo baina ya maeneo ya Oromia na Somali yanayokumbwa na machafuko nchini Ethiopia.