WFP: Matibabu ya utapiamlo yasitishwa nchini Ethiopia kutokana na ukosefu wa fedha
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wiki hii umesimamisha matibabu ya utapiamlo kwa wanawake na watoto 650,000 nchini Ethiopia kutokana na uhaba mkubwa wa fedha. WFP imesema kuwa mamilioni ya watu wako katika hatari ya kukosa misaada.
"WFP linafadhiliwa na nchi 15-20 lakini aghalabu ya nchi hizo ikiwemo Marekani zimepunguza ufadhili mwaka huu", amesema Zlatan Milisic, Mkurugenzi wa Mpango wa Chakula Duniani WFP nchini Ethiopia.
WFP imesema kuwa watu zaidi ya milioni 10 wana upungufu mkubwa wa chakula, ikiwemo milioni 3 waliolazimika kuhama makazi yao kutokana na vita na hali mbaya ya hewa pamoja na wakimbizi kutoka nchi jirani ya Sudan iliyoathiriwa na vita.
Milisic amesema Mpango wa Chakula Duniani tayari umepunguza migao yake ya chakula katika miezi ya karibuni na kwamba oparesheni zake hivi sasa ziko katika hatua mbaya kutokana na ufadhili mdogo.
Wakati huo huo Msemaji wa WFP ameeleza kuwa: Wale wote waliosimamishiwa matibabu ni kutoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikoa ya kaskazini ya Tigray na Afar, na kwamba shirika hilo linatafuta mfadhili ili kununua vifaa na suhula zaidi ili kuanza tena matibabu.
Mgogoro wa chakula nchini Ethiopia umezidi kuwa mbaya katika miaka ya hivi karibuni kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoliathiri eneo la Tigray mwaka 2020 hadi 2022.