UNSC yalaani unyanyasaji wasimamizi wa kusitishwa kwa vita Sudan Kusini
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) limelaani vikali mashambulizi, kuzuiwa na unyanyasaji wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanaosimamia usitishaji vita nchini Sudan Kusini unaofanywa na askari wa serikali.
Wajumbe wa Baraza la Usalama wamesisitiza kuwa unyanyasaji wa wafanyakazi wanaosimamia kusitishwa vita na waangalizi wa Mpango wa Usalama wa Mpito na Utaratibu wa Uthibitisho ulifanyika Jumanne huko Luri, Sudan Kusini, ni ukiukwaji wa makubaliano ya amani.
Wamesema tukio hilo linazua maswali juu ya ahadi ya serikali ya Sudan Kusini ya kuhakikisha jeshi lake linatii makubaliano ya amani. Aidha Baraza la Usalama limeitaka serikali ya Sudan Kusini kuchunguza haraka tukio hilo na kuwawajibisha wote wanaohusika.
Makubaliano ya amani Sudan Kusini yalitiwa saini mwezi Septemba mwaka huu kati ya wawakilishi wa serikali ya Juba na waasi wanaoongozwa na Riek Machar.
Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.