Uchaguzi Mkuu DRC katikati ya changamoto za kiusalama na mivutano ya kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50519-uchaguzi_mkuu_drc_katikati_ya_changamoto_za_kiusalama_na_mivutano_ya_kisiasa
Uchaguzi Mkuu wa Rais na Bunge wa Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo umefanyika leo Jumapili Disemba 30, 2018 huku mvua kali ikinyesha. Uchaguzi huo umefanyika chini ya changamoto nyingi za kiusalama na kisiasa.
(last modified 2025-12-01T10:34:25+00:00 )
Dec 30, 2018 13:40 UTC
  • Uchaguzi Mkuu DRC katikati ya changamoto za kiusalama na mivutano ya kisiasa

Uchaguzi Mkuu wa Rais na Bunge wa Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo umefanyika leo Jumapili Disemba 30, 2018 huku mvua kali ikinyesha. Uchaguzi huo umefanyika chini ya changamoto nyingi za kiusalama na kisiasa.

Hili ni zoezi la kwanza kabisa la kukabidhi madaraka kwa njia ya uchaguzi katika nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika. Rais Joseph Kabila hakuruhusiwa na Katiba kugombea hivyo anatarajiwa kukabidhi madaraka kwa mtu atakayepata kura nyingi kwenye uchaguzi wa leo.

Kabila yuko madarakani Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo tangu mwaka 2001 na ameendelea kutawala hadi hivi sasa baada ya uchaguzi mkuu kuakhirishwa mara kadhaa kwa sababu tofauti.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akipiga kura Jumapili Disemba 30, 2018

 

Vyama vya upinzani vimelalamikia sana uendeshaji wa uchaguzi huo hasa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi CENI kutangaza kutofanyika uchaguzi katika miji mitatu ya Beni, Butembo na Yumbi ambayo ni ngome kuu za wapinzani. Maafisa wa tume hiyo wamedai kuwa, sababu za kiusalama na kiafya hasa kutokana na maeneo hayo kukumbwa na ugonjwa hatari wa Ebola ndizo zilizopelekea kuakhirishwa uchaguzi huo hadi Machi 30, mwakani. Hata hivyo wapinzani wanasema kuwa hivyo ni visingizio tu vya kutaka kuwanyima ushindi wapinzani kwani watu wanaishi kama kawaida katika miji hiyo, wanashiriki katika mikutano ya hadhara na kazi za maofisini na masokoni bila ya hofu yoyote. Miji mbalimbali ukiwemo wa Goma, makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini imeshuhudia maandamano makubwa ya wananchi ya kupinga kuakhirishwa uchaguzi katika miji hiyo mitatu. 

Pamoja na hayo yote, siku chache zilizopita, Rais Joseph Kabila alielezea matumaini yake ya kufanyika uchaguzi huo kama ulivyopangwa. Akihojiwa na televisheni ya al Jazeera ya Qatar, Kabila alisema kuwa hata kama kuna mambo bado hayajakaa sawa kwa ajili ya kufanyika uchaguzi huo katika katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kubwa na pana ya katikati mwa Afrika na licha ya kuweko changamoto nyingi, lakini ana matumaini uchaguzi huo ungelifanyika kama ulivyopangwa.

Kipindi cha pili na cha mwisho cha urais wa Joseph Kabila kilimalizika tarehe 20 Disemba 2016, lakini uchaguzi mkuu uliakhirishwa mara tatu. Mwisho kabisa uchaguzi huo uliakhirishwa tarehe 20 mwezi huu wa Disemba, yaani siku tatu kabla ya tarehe iliyokuwa imepangwa kufanyika kwake, baada ya vifaa vya uchaguzi kuungua kwa moto mjini Kinshasa. 

Martin Fayulu mmoja wa wagombea wakuu wa urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akipiga kura Jumapili Disemba 30, 2018

 

Wakati huo huo Martin Fayulu na Félix Tshisekedi, wagombea wawili wakuu wa upinzani muda mfupi kabla ya kuanza zoezi la kupiga kura leo Jumapili, wamekataa kutia saini hati inayojulikana kwa jina la "Mkataba wa Amani" wakilalamikia kutosikilizwa matakwa yao yakiwemo marekebisho ambayo walipendekeza yafanyike. Hata hivyo, Emmanuel Ramazani Shadary, mgombea wa chama tawala anayeungwa mkono na Rais Joseph Kabila ametia saini hati hiyo. 

Kwa upande wake, Umoja wa Mataifa umetaka uchaguzi huo ufanyike kwa utulivu na amani. Katibu Mkuu wa umoja huo, António Guterres, ametoa taarifa maalumu akizitaka pande zote zinazohusika na uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhakikisha kwamba wananchi wanapiga kura zao katika mazingira ya amani na utulivu kamili.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amewataka viongozi wa kisiasa wa makundi yote, Tume ya Taifa ya Uchaguzi CENI na asasi za kiraia kuhakikisha kunapatikana mazingira yasiyo na machafuko ili watu wote waliotimiza masharti ya kupiga kura, waweze kutumia kwa uhuru haki yao hiyo ya kidemokrasia. Vile vile amewataka wananchi wa Kongo kutumia vyema fursa hiyo ya kihistoria kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura na kuchagua viongozi wanaowataka.

Ikumbukwe kuwa, baada ya Algeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndiyo nchi kubwa zaidi barani Afrika. Ina utajiri mkubwa sana wa maliasili. Hata hivyo kutokana na mizozo ya kisiasa na ukosefu wa utulivu na amani, raia wa nchi hiyo wanaishi katika ukata na umaskini wa kuchupa mipaka.