Watu 10 wauawa kwa shambulio la Daesh kaskazini mashariki mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50520-watu_10_wauawa_kwa_shambulio_la_daesh_kaskazini_mashariki_mwa_nigeria
Raia 10 wameauawa kaskazini mashariki mwa Nigeria kufuatia shambulio la wanamgambo wanaosadikiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 30, 2018 11:06 UTC
  • Watu 10 wauawa kwa shambulio la Daesh kaskazini mashariki mwa Nigeria

Raia 10 wameauawa kaskazini mashariki mwa Nigeria kufuatia shambulio la wanamgambo wanaosadikiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh.

Vyombo vya usalama vimeziambia duru za habari kwamba, mamia ya wakazi wa kijiji kilichoshambuliwa kaskazini mashariki mwa Nigeria wamelazimika kuyahama na kuyakimbia makazi yao baada ya shambulio hilo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, raia hao wamekimbilia katika mji wa Maiduguri ulioko katika jimbo la Borno huko kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuomba hifadhi huko. Ikumbukwe kuwa, jimbo la Borno nalo limekuwa likilengwa kwa mashambulio ya mara kwa mara ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Wakati huo huo, mji wa Buni Gari ulioko katika jimbo la Jobe umekabiliwa na mashambulio ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram. Mashuhuda wanasema kuwa, watu waliokuwa na silaha waliwasili kwa gari katika mji huo na kuanza kuwashambulia kwa risasi raia waliolazimika kukimbia huku na kule kuokoa maisha yao.

Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria

Kundi hilo la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi katika nchi nne zinazopakana na Ziwa Chad za Nigeria, Chad, Niger na Cameroon.

Nchi hizo nne zimeunda kikosi cha pamoja cha kupambana na magaidi wa Boko Haram ingawa hadi hivi sasa zimeshindwa kuliangamiza genge hilo la wakufurishaji. Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria anaendelea kukosolewa kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi yake ya wakati wa kampeni za uchaguzi ya kuliangamiza kundi hilo la kigaidi.