Dec 31, 2018 08:05 UTC
  • Mashindano ya kitaifa ya Qur'ani yafanyika nchini Nigeria

Mashindano ya 33 ya kitaifa ya kila mwaka ya Qur'ani nchini Nigeria yanaendelea kufanyika kwa kushirikisha majimbo 33 ya nchi hiyo katika fani sita za Qur'ani tukufu.

Ibrahim Hassan Dankwambo, Gavana wa jimbo la Gombe, lililoko kaskazini mashariki mwa Nigeria amesema: Mashindano hayo yanaimarisha umoja na maelewano baina ya Waislamu wa nchi hiyo.

Dankwambo ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa kwenye kituo cha Utafiti wa Kiislamu cha Chuo Kikuu cha Usmanu Danfodiyo, mahali yanakofanyika mashindano hayo ya kila mwaka ya Qur'ani katika jimbo hilo la Gombe.

Aidha amewataka vijana wa Kiislamu nchini Nigeria kujifunza kwa pamoja elimu za Kiislamu na za Magharibi ili wawe na nafasi katika maendeleo ya nchi yao.

Abdullahi Abdu Zuru, Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Usmanu Danfodiyo amesema, washindi wa mashindano hayo katika makundi yote mawili ya wanaume na wanawake, wataiwakilisha Nigeria kwenye mashindano ya kimataifa ya Qur'ani yatakayofanyika katika nchi za Saudi Arabia na Kuwait.

Abdullahi Abdu Zuru ameongeza kuwa, Chuo Kikuu cha Usmanu Danfodiyo kinakusudia kuyafanya mashindano hayo msingi mkuu wa mashindano ya Qur'ani ili kuimarisha mafunzo ya Qur'ani nchini Nigeria.

Mashindano ya kitaifa ya Qur'ani Tukufu nchini Nigeria yalianza siku ya Ijumaa ya tarehe 28 Desemba na yataendelea hadi Januari 5 mwaka 2019.../

Tags