Wanajeshi 10 wauawa katika mpaka wa Niger na Nigeria
Siku moja baada ya raia 10 kuuawa kaskazini mashariki mwa Nigeria kufuatia shambulio la kigaidi, askari kumi waliokuwa katika operesheni ya pamoja wameuawa na watu waliokuwa wamebeba silaha katika mpaka wa nchi hiyo na Niger.
Waziri wa Ulinzi wa Niger, Kalla Moutari jana Jumatatu aliliambia shirika la habari la AFP kuwa askari watano wa nchi hiyo na watano wa Nigeria wameuawa katika uvamizi huo, katika eneo la mpakani la Maradi.
Ameongeza kuwa, 'wavamizi' 11 wameuawa pia katika makabiliano hayo ya mwisho wa wiki. Hata hivyo haijabainika iwapo wavamizi hao wana mfungamano wowote na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram au la.
Kundi hilo la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi katika nchi nne zinazopakana na Ziwa Chad za Nigeria, Chad, Niger na Cameroon.
Nchi hizo nne zimeunda kikosi cha pamoja cha kupambana na magaidi wa Boko Haram ingawa hadi hivi sasa zimeshindwa kuliangamiza genge hilo la wakufurishaji.