Jan 02, 2019 02:49 UTC
  • Makundi ya waasi yateka mji wa  Bakouma, Jamhuri ya Afrika ya Kati

Makundi ya waasi yameteka na kudhibiti mji wa Bakouma huko kusini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Ripoti zinasema kuwa, mashambulizi yaliyofanywa na makundi ya waasi ya Muungano wa Amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na Harakati ya Wananchi ya Mapambano yamesababisha hasara kubwa. Taarifa zinasema waasi hao pia wameuteka kikamilifu mji huo na kuchoma moto nyumba na maduka mengi. 

Wakazi wengi wa mji wa  Bakouma wamekimbilia maeneo ya mashambani, vijiji na miji jirani kama ule wa Bangassou ulioko umbali wa kilomita 140 kusini mwa Bakouma.

Siku kadhaa zilizopita wakazi wa mji huo walieleza wasiwasi wao kutokana na kutokuwepo askari wa kulinda eneo hilo na kutahadharisha kuhusu hatari ya mashambulizi ya makundi ya waasi. Vilevile walitoa wito wa kutuma kikosi cha jeshi la taifa katika mji huo na maeneo ya kandokando yake kwa ajili ya kulinda usalama.

Katika miezi ya hivi karibuni maelfu ya raia wamelazimika kukimbia makazi yao katika Jamhuri ya Afrika Kati kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na makundi ya waasi dhidi ya maeneo ya raia. 

Nchi hiyo ilitumbukia katika ghasia na machafuko ya ndani tangu mwaka 2013.     

Tags