Rais wa Nigeria aahidi uchaguzi huru, wapiga kura milioni 84 wasajiliwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50726-rais_wa_nigeria_aahidi_uchaguzi_huru_wapiga_kura_milioni_84_wasajiliwa
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ameahidi kuwa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi ujao utakuwa huru na wa haki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 08, 2019 04:16 UTC
  • Rais wa Nigeria aahidi uchaguzi huru, wapiga kura milioni 84 wasajiliwa

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ameahidi kuwa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi ujao utakuwa huru na wa haki.

Akihutubia mkutano wa chama tawala cha APC mjini Abuja, Rais Buhari amesema uchaguzi wa kuaminika, huru na wa haki ni msingi wa utulivu wa kisiasa na amani kwa nchi yoyote. Ameongeza kuwa tangu mwaka 2015, Tume Huru ya Uchaguzi imeendesha chaguzi za kuaminika kwenye majimbo 195 nchini Nigeria, ambazo zimethibitishwa kuwa bora.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Nigeria, Mahmood Yakubu, amesema watu zaidi ya milioni 84 wamejiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi ujao, idadi ambayo ni asilimia 42 ya wananchi wote, na imeongezeka kwa watu milioni 15.2 ikilinganishwa na ile ya mwaka 2015.

Hayo yanajiri wakati ambao vyama vya upinzani nchini Nigeria vimepinga hatua ya kuteuliwa mtu wa karibu wa familia ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo kuwa ofisa wa ngazi za juu wa Tume ya Uchaguzi, mwezi mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Magaidi wa Boko Haram

Chama cha upinzani cha PDP kimesema uteuzi uliofanywa Alkhamisi iliyopita wa Amina Zakari, mpwa wa Rais Buhari kuongoza moja ya matawi makuu ya Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria (INEC) ni sehemu ya njama za kuandaa mazingira ya kuiba kura katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao wa Februari.

Rais Buhari ambaye aliingia madarakani mwaka 2015 kwa ahadi za kutokomeza ufisadi nchini Nigeria sambamba na kuliangamiza kundi la kigaidi la Boko Haram, amekuwa akikosolewa mno na wapinzani wake kutokana na kile wanachosema kuwa, ameshindwa kutekeleza ahadi zake.