Vyama vinavyomuunga mkono Kabila vyanyakua viti vingi vya Bunge la Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50815-vyama_vinavyomuunga_mkono_kabila_vyanyakua_viti_vingi_vya_bunge_la_kongo_dr
Vyama vya siasa vinavyomuunga mkono rais anayeondoka madarakani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila vimenyakua viti vingi katika uchaguzi wa Bunge.
(last modified 2026-05-19T09:45:50+00:00 )
Jan 12, 2019 04:20 UTC
  • Vyama vinavyomuunga mkono Kabila vyanyakua viti vingi vya Bunge la Kongo DR

Vyama vya siasa vinavyomuunga mkono rais anayeondoka madarakani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila vimenyakua viti vingi katika uchaguzi wa Bunge.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI), vyama hivyo vimenyakua jumla ya viti 288 kati ya 429 Bungeni, huku vyama vya upinzani vikiambulia viti 141 tu.

Kwa mujibu wa sheria, chama au muungano wa vyama unaopata zaidi ya viti 250 ndio wenye sauti na ambao utakuwa na ushawishi wa kulidhibiti Bunge hilo la DRC kwa miaka mitano ijayo. 

Haya yanajiri huku taharuki ikiwa ingali imetanda katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika, wakati huu ambapo Wakongomani wanasubiri kujua muelekeo wa kesi itakayowasilishwa leo hii mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI), Corneil Nangaa

Mgombea wa muungano wa upinzani wa Lamuka katika uchaguzi wa rais Martin Fayulu anadai kuwa yeye ndiye aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo kwa kupata asilimia 61 ya kura, na hii leo anaenda katika Mahakama ya Katiba kupinga matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi yaliyompa ushindi Felix Tshisekedi wa chama cha upinzani cha UDPS.

Kwa mujibu wa CENI, Tshisekedi aliibuka mshindi kwa kuzoa asilimia 38.57 ya kura, Fayulu asilimia 34.8 ya kura, huku Emmanuel Ramazani Shadary aliyewakilisha muungano wa chama tawala akipata asilimia 23.8 ya kura.