Wakimbizi Warundi wanarejea nyumbani, UNCHR yataka misaada zaidi kuwahudumia
Raia wa Burundi waliokimbilia hifadhi katika nchi jirani wameanza kurejea katika nchi yao baada ya kuimarika usalama huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) likotoa wito wa misaada kwa ajili ya kuwasaidia.
Taarifa zinasema wakimbizi kadhaa kutoka Burundi waliopewa hifadhi katika kambi ya Kakuma nchini Kenya wameondoka kurejea makwao.
Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wake limezindua ombi maalumu la kufadhili na kusaidia wakimbizi wa Burundi pamoja na nchi zinazowahifadhi kwa kuzingatia kuwa ufadhili wa mpango huo huchangiwa kwa kiasi kidogo.
Akizungumza Jumanne mjini Geneva, msemaji wa UNCHR Charlie Yaxley amesema UNHCR na washirika wake wanahitaji dola milioni 296 mwaka 2019 kuwasaidia wakimbizi 345,000 kutoka Burundi walio katika nchi jirani. UNCHR inasema wakimbizi wa Burundi ni kati ya waliopuuzwa zaidi duniani.
Kufuatia hali hiyo wakimbizi kutoka Burundi walio katika nchi kama vile Tanzania, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanakabiliwa na hali mbaya sana. Mwaka jana mashirika ya kutoa msaada yalipokea asilimia 35 tu ya dola milioni 391 zilizohitajika kuwasaidia wakimbizi kutoka Burundi.
Mgogoro wa kisiasa Burundi ulianza mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza, kugombea urais katika uchaguzi mkuu kwa mara ya tatu mfululizo, machafuko ambayo yalishika kasi zaidi mjini Bujumbura.
Wapinzani waliitaja hatua ya Rais Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo kwamba, ilikiuka katiba na hati ya makubaliano ya amani ya Arusha Tanzania. Hata hivyo serikali ya Burundi inasisitiza kuwa haijakiuka mapatano ya Arusha.