Jan 16, 2019 16:17 UTC
  • Magaidi wasambaratishwa Dusit Hotel, majeshi ya Kenya yapongezwa

Baada ya Rais Uhuru Kenya wa Kenya kulihutubia Taifa na kutangaza kumalizika shambulizi la kigaidi na utekaji nyara uliodumu kwa muda wa masaa 19 katika Hoteli ya Dusit jijini Nairobi, viongozi mbalimbali wakiwemo wanasiasa wamejitokeza kuvipongeza vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kwa kufanikiwa kuwasambaratisha magaidi hao.

Wakuu wa muungano wa NASA nchini Kenya, Raila Odinga, na Kalonzo Musyoka wameyapongeza majeshi ya Kenya kwa kuwasambaratisha magaidi katika ofisi za Dusit, jijini Nairobi na kufanikiwa kuokoa zaidi ya watu 700 waliokuwa wamezingirwa na magaidi hao. 

Mtandao wa gazeti la Daily Nation umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, katika taarifa yao ya pamoja, viongozi hao ambao walikuwa pamoja na Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu wamesema kuwa, maafisa wa kulinda usalama wa Kenya wametoa majibu mazuri yaliyoratibiwa vyema na kusaidia kuokoa maisha ya watu wengi.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akilihutubia Taifa na kutangaza kusambaratishwa magaidi waliovamia Hoteli ya Dusit jijini Nairobi

 

Raila Odinga amesema: "Tunayashauri majeshi yetu yazidi kuimarisha nguvu zao na kutoa majibu ya haraka na yenye uratibu mzuri zaidi dhidi ya shetani huyu..."

Viongozi hao wameliita shambulio hilo la kigaidi kuwa ni la woga na kuwapongeza Wakenya kwa kuwa kitu kimoja na kujitolea kwa wingi kuchangia damu kwa ajili ya wahanga wa ugaidi huo.

Ingawa katika hotuba yake, Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa, raia 14 wameuawa katika shambulio hilo la kigaidi ambalo genge la ukufurishaji la al Shabab la nchini Somalia limetangaza kuhusika, lakini shirika la habari la Reuters limeinukuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya ikisema kuwa, idadi ya waliouawa imefikia raia 15.

Tags