Ziara ya mabalozi wa Ulaya nchini Libya
-
Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya.
Mabalozi wa nchi za Ufaransa, Uhispania na Uingereza wameelekea nchini Libya kama njia ya kutangaza uungaji mkono wao kwa serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo.
Mabalozi wa nchi hizo tatu muhimu za Ulaya wameelekea mjini Tripoli Libya katika hali ambayo Paolo Gentiloni Silveri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia hivi karibuni naye alifanya ziara nchini Libya. Mabalozi wa Ufaransa, Uhispania ya Uingereza wameonana na Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya katika kambi ya jeshi la majini mjini Tripoli. Katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Waziri Mkuu wa Libya, Fayez al Sarraj aliwataka mabalozi wa nchi za Ulaya wafanye hima ya kurejea haraka nchini Libya. Hizi ni ziara za kwanza za wanadiplomasia wakubwa wa Ulaya kufanywa mjini Tripoli tangu nchi za Ulaya zilipoamua kufunga balozi zao nchini humo katika kipindi cha msimu wa joto kali mwaka 2014. Nchi za Umoja wa Ulaya ziliamua kufunga balozi zao nchini Libya kutokana na nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kukumbwa na fujo na vita vya ndani. Wachambuzi wa mambo ya Libya wanaamini kuwa, licha ya nchi za Ulaya kufunga balozi zao huko Libya, lakini nchi kubwa za bara hilo hazikusita kufuatilia malengo yao haramu nchini humo. Hivi sasa pia kuna uwezekano wa baadhi ya nchi za Magharibi kujiingiza kijeshi nchini Libya. Vitaly Churkin, mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa hivi karibuni aliitahadharisha jamii ya kimataifa juu ya hatua ya nchi za Magharibi ya kufanya mashambulizi ya anga nchini Libya. Matamshi ya mwakilishi huyo wa Russia katika Umoja wa Mataifa yalilenga mashambulizi ya anga ya Marekani ya mwezi Februari mwaka huu wa 2016 ambapo ndege za kivita za Marekani zilishambulia moja ya kambi za mafunzo ya kijeshi za kundi la kigaidi Daesh ndani ya ardhi ya Libya katika mpaka wa nchi hiyo na Tunisia. Naye Jenerali David Rodríguez, kamanda wa askari wa Marekani barani Afrika amesema kuwa mashambulizi ya muungano wa nchi za Magharibi dhidi ya Daesh yataendelea katika maeneo tofauti ya Libya. Itakumbukwa kuwa, Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya aliwasili mjini Tripoli mwezi uliopita wa Machi akiwa pamoja na Baraza lake la Mawaziri akitokea Tunisia. Wakati huo, karibu wabunge 100 wa Libya walitia saini tamko la pamoja la kuinga mkono serikai hiyo ya umoja wa kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa baada ya bunge la Libya kupiga kura ya kutoitambua. Wakati huo huo Spika wa bunge hilo na naibu wake, juzi Jumatano tarehe 13 Aprili walifikia makubaliano ya kuitisha kikao cha bunge ili kulipiga kura Baraza la Mawaziri la serikali hiyo ya umoja wa kitaifa. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, siku ya Jumatatu ya tarehe 18 Aprili, wabunge wa Libya wataipigia kura serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo. Iwapo wabunge 40 watamkataa waziri yeyote yule basi kutakuwa na maana ya kukataliwa waziri huyo na kama mawaziri sita watakosa kura zinazotakiwa kutoka kwa wabunge, basi baraza zima la mawaziri lenye mawaziri 18 litaporomoka. Hii ni katika hali ambayo kabla ya kuwasili mjini Tripol, Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya alikuwa tayari ameshafanya mazungumzo na duru mbalimbali vikiwemo vikosi vya ulinzi na baadhi ya makundi yenye silaha kuhusiana na Baraza la Mawaziri la umoja wa kitaifa. Pamoja na hayo hadi hivi sasa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ina wapinzani wengi kutoka mirengo ya kisiasa. Wapinzani hao wanasema kuwa serikali hiyo ya umoja wa kitaifa si chaguo la wananchi wa Libya, bali imeundwa na wageni. Lililobakia kwa sasa ni kusubiri na kuona wakati utakuja na matunda gani kuhusu mustakbali wa nchi hiyo ya kaskaini mwa Afrika.