Mapigano ya watu wenye silaha yashtadi kaskazini mashariki mwa Nigeria
Makundi yenye silaha yamezidisha mashambulizi yao nchini Nigeria ambapo katika kipindi cha wiki tatu zilizopita zaidi ya askari 100 wa nchi hiyo wameuawa au kutekwa nyara.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetangaza kwamba, mashambulizi ya makundi ya wabeba silaha kaskazini mashariki mwa nchi hiyo yameongezeka sana tangu mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana na kwamba makundi hayo yameweza kudhibiti na kupora idadi kubwa ya silaha na zana zinazomilikiwa na jeshi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ongezeko la mashambulizi ya watu wenye silaha kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika, limepelekea maelfu ya watu kulikimbia eneo hilo na kwenda maeneo mengine yenye amani hususan nchi jirani ya Chad.

Akthari ya mashambulizi hayo yanatekelezwa na wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram lenye mafungamano na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) na ambalo lilianzisha hujuma zake tangu mwaka 2009 nchini Nigeria na katika nchi jirani na taifa hilo. Takwimu zinaonyesha kwamba zaidi ya watu elfu 20 wameuawa, na wengine karibu milioni tatu wamekuwa wakimbizi. Ongezeko la mauaji na mapigano huko kaskazini mashariki mwa Nigeria linajiri katika hali ambayo, uchaguzi wa rais wa nchi hiyo umepangwa kufanyika tarehe 16 Februari mwaka huu ambapo kwa mara ya pili Rais Muhammadu Buhari atagombea kwa muhula wa pili. Mara zote Buhari amekuwa akitoa ahadi za kupambana na machafuko pamoja na ugaidi, ingawa weledi wa mambo wanamtaja rais huyo kuwa aliyefeli katika uwanja huo.