Wahajiri 117 wahofiwa kufa maji katika pwani ya Libya
Wahajiri zaidi ya 100 wanahofiwa kupoteza maisha katika ajali ya kuzama boti katika pwani ya Libya.
Shirika la Kimataifa la Uhajiri IOM lilitangaza jana Jumamosi kuwa, wahajiri 117 ambao Alkhamisi usiku waliondoka mji wa Garabulli ulioko kaskazini magharibi mwa Libya wakiwa na nia ya kufika Ulaya kuomba hifadhi, yumkini wameaga dunia katika bahari ya Mediterania baada ya boti yao ya plastiki kuzama.
Msemaji wa IOM, Flavio Di Giacomo amesema mmoja wa manusura amewaeleza kuwa, walikuwa wahajiri karibu 120 katika boti hiyo, lakini saa 10 au 11 baadaye, chombo hicho dhaifu cha plastiki kilisombwa na mawimbi na kuzama, na watatu tu miongoni mwao ndio wameweza kunusurika.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri IOM, njia ya majini ya kutoka Libya kuelekea nchi za Ulaya ikiwemo Italia na Malta, ndiyo njia hatari zaidi kwa maafa ya roho za watu inayotumiwa na wahajiri waharamu kutoka nchi hasa za Kiafrika kwa safari za kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta maisha mazuri.
Hata hivyo ripoti zinaeleza kuwa asilimia kubwa ya wahajiri hao huwa hawafiki wanakoelekea, bali huishia mikononi mwa magenge ya magendo ya binadamu, kuzama baharini au kupigwa mnada masokoni na kuuzwa kama watumwa.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilitangaza kuwa zaidi ya wahajiri elfu mbili waliaga dunia katika bahari ya Mediterania katika mwaka uliopita wa 2018.