Waislamu Nigeria washinikiza kuachiwa huru mwanahabari Marzieh Hashemi
Waislamu na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Nigeria wamefanya maandamano kulaani kukamatwa na kuwekwa kizuizini nchini Marekani Marzieh Hashemi, mwandishi wa habari na mtangazaji wa kanali ya kimataifa ya Press TV ya Iran.
Wanachama wa Harakati ya Kiislamu Nigeria walifanya maandamano ya amani jana Jumatatu katika mji mkuu Abuja, ambapo wamelaani vikali hatua ya Marekani ya kumkamata Hashemi na kumshikilia korokoroni bila hatia.
Taarifa ya harakati hiyo imesisitiza kuwa, ni kinaya namna Marekani inavyojinadi na kujipiga kifua kuwa ndiye mtetezi nambari moja wa haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari duniani, lakini vyombo vya dola nchini humo vinamzuilia kwa wiki ya pili sasa mwanahabari huyo wa kike Mmarekani mwenye asili ya Afrika, kinyume cha sheria.
Kadhalika waandamanaji na wanaharakati hao wa Nigeria wametaka kuachiwa huru kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye yuko kizuizini tokea tarehe 13 Disemba mwaka 2015.
Jumapili ya tarehe 13 Januari, Marzieh Hashemi, mwenye umri wa miaka 59 alitiwa nguvuni na Polisi ya Upelelezi ya Marekani FBI, ambapo kama ilivyokuwa kawaida yake ya kila baada ya muda, alikuwa amesafiri katika nchi hiyo alikozaliwa ili kwenda kuwatembelea wanawe pamoja na nduyu yake anayeugua.
Wakuu wa Marekani wanamdhalilisha Marzieh Hashemi akiwa korokoroni ikiwa ni pamoja na kumvua hijabu na kumlazimisha ale nyama ya nguruwe ambayo ni haramu kwa Waislamu, kitendo ambacho ni ukiukwaji wa wazi wa matukufu na thamani za Kiislamu.