Nigeria yapinga uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala yake ya ndani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51164-nigeria_yapinga_uingiliaji_wa_nchi_za_kigeni_katika_masuala_yake_ya_ndani
Serikali ya Nigeria imetangaza kuwa, haitakubali uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala yake ya ndani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 27, 2019 23:59 UTC
  • Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria
    Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria

Serikali ya Nigeria imetangaza kuwa, haitakubali uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala yake ya ndani.

Tangazo hilo limetolewa baada ya Umoja wa Ulaya, Marekani na Uingereza kueleza wasiwasi wao kutokana na hatua ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ya kumsimamisha kazi Jaji Mkuu wa nchi hiyo kabla ya uchaguzi muhimu wa rais uliopangwa kufanyika mwezi ujao.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, Garba Shehu imesema kuwa: Serikali ya Abuja itahakikisha uchaguzi ujao unafanyika kwa uhuru na uadilifu na haitaziruhusu nchi za kigeni kuingilia mambo yake ya ndani.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, Nigeria haitakubali aina yoyote ya uingiliaji au mitazamo inayoeneza shaka na wasiwasi kuhusu matokeo ya uchaguzi ujao.

Mpinzani mkuu wa Buhari katika uchaguzi ujao wa rais, Abubakar Atiku (kushoto)

Siku chache zilizopita Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria alimsimamisha kazi Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Walter Onnoghen, hatua ambayo inahusishwa na uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 16 mwezi ujao wa Februari.

Jaji Mkuu nchini Nigeria ni Rais wa Mahakama ya Juu yenye jukumu la kusikiliza kesi ya kupinga ushindi wa matokeo ya urais.

Timu ya wasimamizi wa uchaguzi ya Umoja wa Ulaya imepinga hatua hiyo na kusisitiza kuwa inazusha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutotendeka haki na uadilifu katika uchaguzi ujao.

Vilevile vyama vya upinzani nchini Nigeria vimesimamisha kampeni za uchaguzi kwa muda wa masaa 72 kulalamikia hatua ya serikali ya Rais Muhammadu Buhari ya kumsimamisha kazi Jaji Mkuu wa nchi hiyo.

Mkuu cha chama cha upinzani cha Peoples Democratic Party, Atiku Abubakar ameuataja uamuzi huo wa Ijumaa iliyopita kuwa ni udikteta wa kupindukia. Amesema, "Huu ni muendelezo wa ubakaji wa demokrasia iliyopiganiwa kwa jitihada kubwa."