Jenerali Haftar atangaza marufuku ya kuruka ndege kusini mwa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51440-jenerali_haftar_atangaza_marufuku_ya_kuruka_ndege_kusini_mwa_libya
Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar limetangaza kuwa ni marufuku kuruka ndege katika anga ya kusini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 09, 2019 12:31 UTC
  • Jenerali Haftar atangaza marufuku ya kuruka ndege kusini mwa Libya

Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar limetangaza kuwa ni marufuku kuruka ndege katika anga ya kusini mwa nchi hiyo.

Vikosi vya Jeshi la Taifa la Libya vimetangaza marufuku kuruka ndege katika anga ya kusini mwa nchi hiyo sambamba na kushadidi mapigano ya kuwania udhibiti wa medani kubwa zaidi ya mafuta katika eneo hilo.  

Kamanda wa oparesheni ya kikosi cha anga cha Jeshi la Taifa la Libya ametangaza kuwa, ni marufuku kuruka ndege yoyote katika anga ya kusini mwa nchi hiyo bila ya kuwa na kibali na hakuna ndege yenye haki ya kutua kwenye viwanja vya ndege vya kusini mwa Libya. Wanajeshi hao wanaoongozwa na Jenerali Haftar wametahadharisha kuwa, ndege yoyote itakayopuuza tahadhari hiyo itakabiliwa na hatari na inaweza kutunguliwa. 

Jenerali Khalifa Haftar
 

Jeshi la Taifa la Libya limesema kuwa, limechukua uamuzi huo likihofia kuwepo uwezekano wa kutumwa silaha kwa wanamgambo wa Chad katika eneo hilo.

Mwezi uliopita wa Januari Jeshi la Taifa ya Libya lilianzisha oparesheni kubwa kusini magharibi mwa nchi hiyo kwa lengo la kuwasaka magaidi.