Tundu Lissu atakiwa na Waziri Lugola kurejea Tanzania ili kusaidia upelelezi
(last modified Thu, 14 Feb 2019 08:11:04 GMT )
Feb 14, 2019 08:11 UTC
  • Tundu Lissu atakiwa na Waziri Lugola kurejea Tanzania ili kusaidia upelelezi

Wakati Tundu Lissu Mbunge wa upinzani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania akiendelea na ziara zake nchini Marekani, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Kangi Lugola amemtaka mwanasiasa huyo kurejea nchini ili kusaidia upelelezi wa tukio lake la kushambuliwa kwa risasi.

Akizungumza na waandishi wa habari  hapo jana mjini Arusha kaskazini mwa Tanzania, Waziri Lugola amesema kuwa, Lissu ndio mwenye kesi hiyo, Serikali inashindwa kuendelea na upelelezi wa tukio la kushambuliwa kwake kwa sababu haina mashahidi muhimu."

Hata hivyo Tundu Lissu mwenyewe amekuwa akikosoa kauli kama hizo za kukwama upepelezi mpaka arejee akihoji kwamba, kama angeuawa katika shambulio hilo ina maana upepelezi usingefanyika kwa kutokuweko yeye?

Tundu Lissu, Mbunge wa upinzani ambaye amekuwa akiikosoa vikali serikali ya Rais Magufuli

Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi mnamo Septemba 7 mwaka 2017 na watu wasiojulikana akiwa mjini Dodoma na kisha baadae kupelekwa Nairobi, Kenya kwa ajili ya matibabu ambapo huko alifanyiwa oparesheni kadhaa na mwishowe kupelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Serikali ya Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kulaumiwa na vyama vya upinzani na asasi za kutetea haki za binadamu nchini humo kutokana na kupiga marufuku maandamano hatua ambayo inatajwa kuwa ni kukandamiza demokrasia.

Hata hivyo serikali ya Rais Magufuli imekuwa ikitetea kwa kusema kuwa, maandamano yamekuwa yakihatarisha amani ya nchi hiyo hasa kutokana na wanasiasa wa upinzani kutumia majukwaa ya kisiasa na maandamano kutoa maneno ya kichochezi.