Nigeria yaakhirisha ghafla uchaguzi wa rais
Tume ya Uchaguzi nchini Nigeria imeakhirisha kwa wiki moja uchaguzi mkuu uliotazamiwa kufanyika hii leo.
Mahmood Yakubu, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria INEC ametoa tangazo hilo la ghafla masaa machache kabla ya wananchi wa Nigeria kuelekea katika masanduku ya kupiga kura kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia.
Amesema uchaguzi huo umeakhirishwa kwa sababu za kilojistiki, akisisitiza kuwa tume hiyo ina nia ya kuendesha uchaguzi huru, wa haki na kuaminika.
Kuna wapiga kura zaidi ya milioni 84 katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika yenye utajiri wa mafuta.
Katika uchaguzi huo ambao sasa utafanyika Februari 23, Wanigeria wanatazamiwa kupiga kura kuchagua kati ya Rais wa sasa Muhammadu Buhari anayewania muhula wa pili au mmoja kati ya wagombea wengine 72 ambao wanataka kumng'oa madarakani kiongozi huyo.
Hata hivyo mfanyabiashara Atiku Abubakar wa chama cha upinzani cha PDP ndiye anayetazamiwa kuchuana vikali na Buhari katika kinyang'anyiro hicho.