Idadi ya waliouawa katika shambulizi la wabeba silaha Nigeria yapindukia 130
Gavana wa jimbo la Kaduna lililoko kaskazini magharibi mwa Nigeria amesema idadi ya watu waliouawa katika shambulizi la watu wenye silaha Ijumaa iliyopita imeongezeka maradufu.
Nasir el-Rufai aliyasema hayo jana mjini Abuja na kuongeza kuwa, polisi inachunguza lengo la shambulizi hilo lililofanyika siku moja kabla ya uchaguzi ulioakhirishwa na kuua watu 130.
Amesisitiza kuwa, hakuna ishara yoyote kuwa shambulizi hilo lilikuwa na mfungamano na uchaguzi huo.
Duru za habari zinasema yumkini mauaji hayo yalikuwa ya kikabila.
Uchaguzi mkuu nchini Nigeria ulikuwa ufanyike Jumamosi iliyopita lakini ukaakhirishwa ghafla na Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria INEC, ambayo ilitangaza kuwa sasa utafanyika Februari 23.
Hii ni katika hali ambayo, kundi la wanamgambo linalojiita Walipizaji Kisasi wa Delta (Delta Avengers) linaloendesha harakati zake katika eneo lenye utajiri wa mafuta la Niger Delta kusini mwa Nigeria limetishia kuwa litausambaratisha na kuulemaza uchumi wa nchi hiyo endapo Rais Muhammadu Buhari atachaguliwa tena katika uchaguzi utakaofanyika siku ya Jumamosi.